
Hali
za majeruhi wa ajali iliyohusisha basi dogo la abiria eneo la
Makunganya, barabara kuu ya Morogoro-Dodoma lililokuwa na mashabiki wa
timu ya Simba, zinaendelea vizuri, huku majeruhi mmoja akihamishiwa wodi
ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Aidha,
miili ya watu watano kati ya saba imeshatambuliwa, ukiwemo mwili wa
Abdala Fundi, Abdala Uwadi, Nurdini Mayopa, Rehema Musa na Ramadhani
Kingolini maarufu kama Ngumi Jiwe.
Mganga
mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Ritta Lyamuya,
alisema ajali hiyo iliyotokea juzi usiku, walipokea majeruhi 23, ambapo
wawili walifariki dunia wakipatiwa matibabu na watu watano waliopoteza
maisha eneo la ajali.
Dk.
Lyamuya alipongeza jitihada zilizofanywa na Mbunge wa Morogoro Mjini,
Abdulaziz Abood, kwa msaada wa vifaa tiba, mara tu baada ya ajali, jambo
lililoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma hospitalini hapo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema chanzo cha ajali
hiyo ni dereva wa gari hiyo kukosa umakini na kutokuwa na uzoefu wa
barabara hiyo, ambayo imekuwa na utelezi katika eneo hilo mvua
zinaponyesha, na kuwataka madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za
usalama barabarani.
Abiria
walionusurika katika ajali hiyo, walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni
utelezi uliosababishwa na mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha,
uliomfanya dereva wa gari waliyokuwa wamepanda aina ya costa, yenye
namba za usajili T 304 CWN kushindwa kumudu na kuserereka kwa umbali
mrefu, kabla ya kupinduka na kukwama kwenye ukingo wa barabara.
0 comments:
Post a Comment